Thursday , 17th Jan , 2019

Mwandishi wa habari za uchunguzi ambaye aliripoti habari ya rushwa kwenye soka nchini Ghana, Ahmed Hussein-Suale, ameuawa kwa kupigwa risasi usiku wa Jumatano ya Januari 16.

Jeshi la Polisi nchini Ghana limesema kwamba Ahmed alipigwa risasi mara mbili na kufariki wakati akiwa njiani kuelekea hospitali.

Taarifa zaidi zinasema kwamba Ahmed alikuwa njiani akielekea nyumbani kwake, na ndipo walipojitokeza watu wawili wakiwa kwenye pikipiki na kumpiga risasi kisha kukimbia.

Mwandishi huyo alijizolea umaarufu nchini Ghana na Afrika kwa ujumla, kutokana na kufichua siri nyingi juu ya kukithiri kwa rushwa kwenye soka barani Afrika, ikiwemo aliyekuwa Rais wa Chama cha Soka Nchini Ghana GFA, kwesi nyantakyi mwezi Oktoba mwaka uliopita.