Friday , 10th Mar , 2017

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limezitakia la kheri timu za Tanzania, Young Africans na Azam FC ambazo zina mechi za kimataifa zitakazofanyika Jumamosi na JUmapili wiki hii.

 

Maandalizi yote yamekamilika ambako Young Africans dhidi ya Zanaco, zitacheza kesho Jumamosi Machi 11, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.00 jioni. Waamuzi kutoka Djibouti ndio watakaochezesha mechi hiyo.

Waamuzi hao ni Djamal Aden Abdi ambaye atapuliza kipenga wakati wasaidizi wake ni Hassan Yacin na Farhan Salime ilihali mwamuzi wa akiba atakuwa Souleiman Djamal. Kamisha katika mchezo huo Na. 61 atakuwa Luleseged Asfaw kutoka Ethiopia.

Kiingilio katika mchezo huo kwa mujibu wa Mratibu wa Mechi za Kimataifa wa Young Africans, Mike Mike ni Sh 20,000 kwa VIP ‘A’, Sh 10,000 kwa VIP ‘B’ na ‘C’ na Mzunguko (Viti vya Rangi ya chungwa, kijani na bluu) ni Sh 3,000.

Azam wao watacheza Jumapili Machi 12, mwaka huu na Mbabane Swallows ya Swaziland kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam.  

Waamuzi watakochezesha mchezo huo wanatoka Benin ambao ni Mwamuzi wa kati, Addissa Abdul Ligali na wasaidizi ni Medegnonwa Romains Agbodjogbe na Babadjide Bienvenu Dina huku Mwamuzi wa akiba akiwa Moumouni Kiagou na kamisha wa mchezo atakuwa Mohamed Omar Yusud wa Kenya.

Kiingilio katika mchezo huo kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba ni Sh 10,000 kwa VIP, Jukwa Kuu itakuwa ni Sh 5,000 na Mzunguko itakuwa ni Sh 3,000.