Friday , 2nd Aug , 2019

Katika mwendelezo wa kuhakikisha wasichana wanaongeza ufaulu katika masomo yao, Kampeni ya Namthamini inayoendeshwa na East Africa Television na East Africa Radio, iliweka kambi ya wiki moja katika mikoa ya Arusha na Manyara kwaajili ya kugawa taulo za kike wa wanafunzi.

Kampeni hiyo imepita katika shule tano, mbili zikiwa ni shule za Sekondari Simbay na Sumaye, zilizopo Wilaya ya Hanang mkoani Manyara, ambapo Mkuu wa Wilaya hiyo Joseph Mkirikiti, aliungana na timu ya Namthamini kutoka East Africa Television na East Africa Radio kwenye zoezi la ugawaji wa taulo hizo.

Jumla ya wasichana 300 katika shule hizo walipata taulo za kike zitakazowatosha kwa mwaka mzima.

Kwa upande Mwingine mkoa wa Arusha katika Wilaya za Arusha Mjini na Arumeru, nazo zilinufaika na Namthamini kwa mwaka 2019. Jumla ya wasichana 300 walipata taulo hizo katika shule za sekondari Muriet na Kinana ambapo Afisa Elimu Taaluma Sekondari mkoa wa Arusha Kabesi Kabeja, alishuhudia zoezi hilo.

Pia timu ya Namthamini kwa kushirikiana na Afisa Elimu Taaluma Sekondari mkoa wa Arusha Kabesi Kabeja, ilisafiri umbali wa Kilometa 25, kutoka Arusha Mjini hadi Arumeru ilipo shule ya sekondari Musa na kukabidhi taulo za kike kwa wanafunzi zaidi ya 200.

Kampeni ya Namthamini kupitia East Africa Television na East Africa Radio, imeendelea kwa mwaka wa tatu sasa, ambapo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaochangia taulo za kike, imefanikiwa kuwafikia wanafunzi zaidi ya 3000 nchi nzima.