Thursday , 15th Aug , 2019

Mkuu wa mkoa wa Tabora Mh. Aggrey Mwanri, ameipokea kampeni ya Namthamini ya East Africa Television na East Africa Radio, ambayo imefanikisha wasichana zaidi ya 1000 kubaki shuleni kwa mwaka mzima kwa kuwapatia taulo za kike.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akipokea taulo za kike kwaajili ya wanafunzi wa shule ya sekondari Ndono.

Akiongea leo Agosti 14, 2019 kwenye zoezi la ugawaji wa taulo za kike katika shule ya sekondari Ndono iliyopo wilayani Uyui, Mwanri amesema kitendao cha East Africa Television na East Africa Radio kupitia kampeni ya Namthamini, kupeleka pedi mkoani Tabora kimeweka alama ya kudumu.

''East Africa Television na East Africa Radio mmepiga mhuri katika mioyo ya watu wa Tabora, hatutakaa tusahau hili jambo mlilolifanya hapa'' - Mh Aggrey Mwanri Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

Aidha Mkuu huyo wa mkoa ameiunga mkono kampeni ya Namthamini kwa kutoa kiasi cha shilingi Mil 1, kwaajili ya kuongeza taulo hizo katika shule za Ndono na Idete zote za wilayani Uyui.

Shule hizi mbili ni sehemu ya shule 4 zitakazopata pedi za kutosha wanafunzi kwa mwaka mzima mkoani Tabora. Huu ni mwendelezo wa zoezi la ugawaji wa Pedi hizo baada ya kuanza katika mikoa ya Arusha na Manyara.

Ikumbukwe kuwa kampeni ya Namthamini inaendelea kwa mwaka wa tatu sasa, na tayari imeshagusa maisha ya wanafunzi wa kike zaidi ya 5000 kote nchini.