Tuesday , 8th Dec , 2020

Michuano ya ligi ya mabingwa barani ulaya inatazamiwa kuendelea tena usiku wa hii leo kwa michezo nane ya mzunguko wa 6 na wa mwisho wa hatua ya makundi ili kutafuta vilabu 16 zitakavyofuzu kutinga hatua inayofuata ya 16 bora itakayochezwa mapema mwaka 2021.

Manchester United wanahitaji sare tu, dhidi ya Rb Leipzing usiku wa leo ili kujihakikishia nafasi hatua ya 16 bora ligi ya mabingwa ulaya

Macho na Masikio ya wapenzi na wafuatiliaji wa soka ulimwenguni yameelekezwa kwenye michezo miwili kutoka kundi H lenye timu za Man Utd ambaye ni kinara, PSG, RB Leipzig wote watatu wakiwa na alama sawa alama 9 na Instanbul Basaksekhir anayeshika mkia akiwa na alama 3 pekee.

Vinara wa kundi hilo Man Utd wamesafiri kutoka Uingereza kuwafuata RB Leipzig Nchini ya Ujerumani ili kusaka alama 3 ama alama 1 ili kufuzu hatua ya 16 bora ilhali RB Leipzig na wao wakisaka ushindi ama alama 1 ili waweze kufuzu na kuweka rekodi ya kufuzu mara 2 mfululizo hii ni endapo PSG atapoteza mchezo wake dhidi Basaksekhiri.

Kuelekea kwenye mchezo huo kocha wa Man Utd Ole Gunnar Solskjear amethibitisha kuwa washambuliaji wake Edinson Cavani na Anthony Martial watakosekana kufuatia majeraha waliyoyapata mchezo uliopita dhidi ya Westham United.

Kwa Upande wa wenyeji wa mchezo huo RB Leipzig wao wanatazamiwa kumkosa mlinzi wao wakutegemewa Dayot Upamecano anayetumikia adhabu ya kuoneshwa kadi za njano mfululizo pamoja na Lazar Samardzic mwenye maambukizi ya ugonjwa wa Korona.

PSG matajiri wa jiji la Paris nchini Ufaransa watawakaribisha Instanbul Basaksekhir ya nchini Uturuki wakiwa kwenye dimba la parc de prince wakijiandaa kupambana kusuka ama kunyoa, kupata ushindi ili kusonga mbele ama kupata sare na kuombea Man Utd wawafunge RB Leipzig ili wafuzu 16 bora.

Michezo mingine inayotazamiwa kuchezwa hii leo ni, Lazio dhidi ya Clubb Brugge na Zenit St.Petersburg zote kuchezwa saa 2:55 Usiku. Barcelona dhidi ya Juventus, Dynamo Kiev kucheza na Ferencovaros, Chelsea dhidi ya Krasnodar wakati Sevilla na Rennes zote saa 5 Usiku Afrika Mashariki.