Wednesday , 30th Dec , 2020

Wekundu wa Msimbazi Simba SC ambao ndiyo mabingwa watetezi wa VPL saa 10:00 jioni ya leo Disemba 30, 2020, wanatazamiwa kukipiga dhidi ya klabu ya Ihefu FC ya Jijini Mbeya mchezo utakaochezwa kwenye dimba la Mkapa jijini Dar es salaam.

Wachezaji wa Simba SC

Kuelekea kwenye mchezo huo Simba inatarajia kumkosa kiungo wake Jonas Mkude, ambaye ametangazwa kusimamishwa na klabu hiyo kwa muda usiojulikana kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu zinazomkabiri klabuni hapo.

Nahodha wa wekundu wa msimbazi John Bocco huenda akakosekana kutokana na kuwa na majeraha ambayo yalimuweka nje kwenye mchezo ambao Simba walicheza na FC Platinum ya Zimbabwe, juma lililopita kwenye mchezo wa kuwania kufuzu makundi klabu bingwa Afrika.

Mchezo huo ambao ni wa kwanza kwa wawili hao kwenye mzunguko wa pili, unatazamiwa kuwa wa ushindani kutokana na Simba kutaka kupunguza utofauti wa alama 11 na kinara Yanga licha ya kuwa nyuma ya michezo 3 ilhali Ihefu ikiendelea kuimarika chini ya kocha wake Zuberi Katwila.

Tokea Zuberi Katwila atue Ihefu Oktoba 18, ameiongoza klabu hiyo kwenye michezo 11 akishinda 2, kupoteza 5 na kutoa sare michezo 4 ikiwemo kufungwa na Yanga pekee kwenye michezo yake 4 ya mwisho na kujikusanyia alama 13 zilizofufua matumaini ya kusalia VPL.

Ihefu ambayo ni klabu changa, imekutana na Simba kwenye VPL mara moja kwenye mchezo wa kwanza wa VPL ambapo Simba waliifunga Ihefu mabao 2-1 kwenye mchezo uliokuwa na upinzani mkali.