Tuesday , 19th Jan , 2021

Msanii wa Bongofleva Alikiba amesema moja ya sababu kubwa ya kuimba kwa lugha ya kifaransa kwenye ngoma yake mpya Infidele ni kutokana na lugha hiyo kutumiwa na watu wengine duniani hivyo kuna uwezekano wa muziki wake kuwafikia watu wengi.

Alikiba

Alikiba amefunguka hilo leo Januari 19, 2021 kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, ambayo huruka Jumatatu mpaka Ijumaa saa 7:00 mchana hadi saa 10:00 jioni.

''Nilifikiria tu kuwa jamii ya watu wengi duniani wanaongea kifaransa hivyo nikaona ni jambo zuri, japo kwenye matamshi ilikuwa kazi kubwa sana na nitoe shukrani kwa msichana mmoja anaitwa Aaliyah, wakati nikiwa Afrika Kusini naandika huu wimbo alinisaidia sana'', amesema Alikiba.

Aidha amekiri kuwa yeye sio mtalaam sana wa lugha hiyo lakini amekuwa akijifunza taratibu na sasa ameelewa hata matamshi hayamsumbui sana. Lakini pia ameelezea maana ya kifaransa alichoimba.

''Kiukweli mimi sio mfaransa ila nimejifunza, nilichoimba kwenye kipande cha kifaransa ni kama marudio tu ya verse ya kwanza ila imebadilika lugha tu, lakini ujumbe ni ule ule'', amefunguka Alikiba.

Jana Jumatatu Januari 18, 2021, mwimbaji huyo aliachia ngoma yake mpya inayoitwa Infidele ambayo ndani ameimba baadhi ya mashairi kwa lugha ya kifaransa.