Friday , 29th Jan , 2021

Kocha wa Klabu ya Tottenham Hotspurs, Jose Mourinho amethibitisha kwamba atamkosa mshambuliaji wake matata, Harry Kane kwa majuma machache kufuatia kupata majeraha ya kiundo cha mguu katika mchezo wa jana dhidi ya Liverpool.

Nahodha wa Tottenham Hotspurs, Harry Kane akiugulia maumivu katika mchezo wao dhidi ya Liverpool

Kane ambaye ni nahodha wa Spurs alipata maumivu alipogongana na Thiago Alcantara na baadae dhidi ya Jordan Handerson na ililazimika atolewe kikosini baada ya kipindi cha kwanza kumalizika katika mchezo ambao timu yake ilifungwa na Liverpool bao 3-1.

''Harry Kane aliondoka uwanjani lakini akiwa anahitaji kuendelea na mchezo, sidhani kama angeumia sana angetaka kucheza, ingawa inabidi tusubiri ripoti ya matabibu lakini ninaamini hatokaa nje kwa muda mrefu'' alisema Kocha Jose Mourinho.

Nyota huyo raia wa Uingereza, alikosekana katika michezo tisa ya msimu uliopita baada ya kupata majeraha ya misuli ya paja, lakini tangu arejee msimu huu amefanikiwa kucheza katika mechi zote 19,na ndiye kinara kwa kupachika mabao kwenye EPL akiwa na mabao 12.

Tottenham ilipoteza nafasi ya kushinda ambayo ingesogea hadi ndani ya nne bora katika msimamo wa ligi na sasa wameendelea kusalia nafasi ya sita kwa alama zao 33 huku Liverpool ikisogea hadi nafasi ya nne wakiwa na alama 37.