Saturday , 4th Sep , 2021

Kocha wa Kagera Sugar, Francis Baraza amesema sasa amebaini kuwa vilabu vya Yanga, Simba na Azam vipo sahihi kusajili wachezaji wengi wa kigeni kwakuwa asilimia kubwa ya wazawa wanacheza mpira kwa mazoea.

Kocha Francis Baraza akiwa mazoezini na kikosi chake cha Kagera Sugar kinachojiwinda na msimu mpya wa mashindano.

Raia huyo wa Kenya anayewania tuzo ya Kocha bora wa msimu uliopita, ameyasema hayo baada ya kuwakosa wachezaji takribani 15 kambini licha ya kuwapa taarifa lakini bado hawaungana na wenzao jambo linalompa ugumu kuiandaa timu yake kuelekea msimu ujao.

''Nimesajili wachezaji wanne wa kigeni kwasababu nataka tuwape changamoto wachezaji wazawa, bahati mbaya asilimia kubwa wanacheza mpira kwa mazoea ingawa wanavipaji vikubwa, inawezekana labda hawana misingi kuanzia kwenye shule za soka''

''Mpaka sasa ninawakosa wachezaji 15, na taarifa wanayo lakini hawajafika, inanipa ugumu kuiandaa timu lakini hakuna shaka nitatumia vijana siwezi kushindwa''

Katika hatua nyingine kocha huyo wa zamani wa Biashara Mara United amesema kwake hakuna mchezaji wa kigeni atakayekaa benchi kwani anaamini wanatambua kazi yao ndio maana hawachelewi kufika kambini.

Kumekuwa na mjadala wa muda mrefu juu ya ongezeko la idadi ya wachezaji wa kigeni katika vilabu kutoka 10 hadi 12 wengi wakiamini ni kuwanyima fursa wazawa lakini wengine wakisema kuwa ni kuwajengea ushindani utakaoboresha Ligi yetu kuwa bora zaidi Afrika.