
Makamu wa Rais wa BFT, Donath Massawe wa shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (OBFT)
Ameyasema hayo leo Mei 23, 2022 Makamu wa Rais wa BFT, Donath Massawe wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliokuwa na lengo la kuwataarifu watanzania kuhusu mashindano ya kimataifa ya majaribio yanayotarajiwa kufanyika kwa siku 5 kuanzia Mei 27 hadi 31 Jijini Dar es salaam, kuwaandaa mabondia kimataifa kabla ya kushiriki katika michezo hiyo ya Burmgham nchini Uingereza.
"Tukiwa kambini wakati wa mafunzo mara nyingi tunawahasisha mabondia waendelee kujituma na kuonesha viwango vizuri ili kuifanya Serikali iwe na moyo wa kusaidia michezo zaidi,"alisema Massawe.
Alisema kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefadhili kwa asilimia 100 maandalizi yote ya timu zote, hivyo inawalazimu kuonyesha kile kilichofadhiliwa kimelipwa kwa njia moja ama nyingine.
"Mimi nawahakikishia watanzania waamini kwamba tukienda huko hatutarudi bila medali ,"alisisitiza Massawe.
Wakati huo huo aliendelea kuwaomba watanzania kujitokeza katika mashindano hayo ili kuwapa motisha mabondia kujituma zaidi huku akieleza kuwa, mashindano hayo yatakuwa chachu ya wanamichezo na mabondia kujituma zaidi.
Naye Katibu Mkuu Msaidizi wa OBFT Mohamed Abubakari ,alisema kuwa timu inaendelea na kambi hadi itakapokwenda kushiriki mashindano hayo ya Jumuiya ya Madola.
Alisema kuwa vijana wapo katika hali nzuri na wana morali ya kuhakikisha wanafanya vyema na hakuna majeruhi.
"Mashindano yetu ambayo tutaanza Mei 27 -31 yataendeshwa kwa mfumo wa ligi na nchi ambazo tumezialika wanakuja na uzito wa mabondia wetu, hivyo watapambana na mabondia wa uwezo tofauti tofauti" amesema Mohamed.
Mashindano hayo yatashirikisha nchi zaidi ya 6 za Afrika ikiwemo Malawi, Zambia, Msumbiji, Sudani Kusini, Uganda, Swaziland na wenyeji Tanzania.