Thursday , 4th Aug , 2022

Mwanariadha wa Kenya wa mbio fupi za mita mia moja Ferdinand Omanyala ameushangaza ulimwengu baada ya kuibuka mshindi na kutwaa medali ya dhahabu katika michezo ya nchi za Jumuiya ya Madola inayoendelea mjini Birmingham nchini Uingereza.

Ferdinand Omanyala mwanariadha wa Kenya- mbio fupi za mita mia moja.

Omanyala alimaliza mbio hizo kwa kumia muda wa sekunde kumi na nukta mbili na kuipatia Kenya medali ya kwanza ya dhahabu katika michuano hiyo baada ya kumshinda bingwa mtetezi wa mbio hizo Akani Simbine kutoka Afrika Kusini aliyemaliza katika nafasi ya pili.

(Bondia wa Tanzania Yusuf Changalawe (kulia) akinyanyuliwa mkono juu baada ya kushinda pambano)

Upande mwingine Tanzania imejihakikishia medali ya pili kwenye michuano hiyo baada ya bondia Yusuf Changalawe kumchapa kwa knockout bondia Arthur Langlier wa St. Lucia na kutinga nusu fainali kwenye mchezo wa ngumi za ridhaa za uzani wa juu wa kati (light heavyweight).

Kwa maana hiyo hata kama Changalawe atapoteza pambano la nusu fainali, bado atatunukiwa medali shaba kwa mujibu na kanuni za ngumi za ridhaa, kwani kanuni zao zinawatambua mabondia walioshindwa kwenye nusu fainali kuwa ni washindi watatu, huku wale walioshinda wataingia fainali ili kupata bingwa na mshindi wa pili.