Monday , 28th Nov , 2022

Wavuvi 70 wakiwemo walioshiriki kuokoa watu kwenye ajali ya ndege iliyozama ziwa Victoria Novemba 06/2022 wameanza kupatiwa mafunzo maalumu ya ukoaji kutoka idara ya maafa ofisi ya Waziri Mkuu, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kushiriki uokoaji pindi zitakapotokea ajali

Kutolewa kwa mafunzo hayo ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alilolitoa wakati wa ajali hiyo akiwa mkoani Kagera

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo ambayo yamewashirikisha wavuvi hao kutoka wilaya za Missenyi na Bukoba, Mkurugenzi msaidizi Idara ya maafa ofisi ya waziri mkuu, Luteni Kanali Selestine Masalamado amesema kuwa mafunzo hayo pia yatawawezesha wavuvi hao kutoa taarifa sahihi na kwa wakati, ili kupunguza madhara yanayoweza kutokea.

Novemba 06 mwaka huu ndege ya shirika la Precision Air ilidondoka katika ziwa Victoria na kusababisha vifo vya watu 19, huku wengine 26 wakiokolewa, miongoni mwao wakiwamo watu 24 waliokuwa abiria katika ndege hiyo.