Wednesday , 28th Dec , 2022

Kiasi cha Tsh. milioni 10 kimetolewa na Umoja wa wanakyela waishio ndani na nje ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya mwaka 2022  kwa ajili ya kuwapatia bima za Afya iliyoboreshwa kaya 60 zenye watu 300, vifaa tiba  na madawati 30.

Ni miaka minne sasa umoja  huo umekuwa ukitoa msaada wa vitu mbalimbali katika sekta ya Afya na Elimu kila ifikapo mwisho wa mwaka ikiwa ni utaratibu wa kuhamasishana wanakyela kurudi nyumbani.

Mpaka sasa zaidi ya wananchi 1000 wamepatiwa bima za Afya iliyoboreshwa ambapo wanapata huduma za matibabu bure kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Mwenyekiti wa Ibhasa Group Festival, Yessaya Mwakifulefule amesema wameshawishiwa kufanya hivyo ikiwa ni sehemu ya kurudisha fadhila walipotoka.

“Tunajivunia kuwa sehemu ya mafanikio wilayani kwetu hapa Kyela huu ni mwaka wa nne sasa kila ikifika desemba wanakyela waishio maeneo mbalimbali wanarudi kwa ajili ya kutoa misaada ya vitu mbalimbali ili kuboresha sekta ya Afya na Elimu pamoja na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja kupitia matamasha yaliyoandaliwa, amesema Mwakifulefule. 
 Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye Ulemavu wilayani Kyela Chawata, David Mwakitalu amesema ni nadra watu waliofanikiwa kukumbuka kwao na kutoa misaada ya aina mbalimbali.

Alisema bima hizo za Afya zimegusa maisha yao moja kwani sasa watakuwa na uhakika wa matibabu kuliko ilivyokuwa Mwanzo.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Mariam Ngwere amesema msaada huo wa bima za Afya na vifaa ya matibabu ikiwemo vya kujifungulia na upasuaji vitaisaidia Serikali kupunguza gharama za ununuzi wa vifaa hivyo.

Amewaomba kuendelea kuwasaidia katika sekta ya afya kwani mahitaji bado ni makubwa  likiwemo suala la utoaji wa bima za Afya.

Umoja wa Ibhasa Festival umekuwa ni msaada mkubwa kwa Wilaya ya Kyela katika kuleta maendeleo, mpaka miongoni mwa mafanikio ni kuchangia ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambayo ujenzi wake umefikia hatua nzuri.