Wednesday , 1st Feb , 2023

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) haijazuia vibali vya kukamilisha miradi ya kimkakati ya kupeleka umeme vijijini kwa kupitisha nguzo za umeme katika hifadhi za misitu nchini.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja

Ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu aliyetaka kujua mikakati ya serikali ya kutochelewesha vibali vya kuruhusu umeme kupita kwenye hifadhi za misitu ili kuwahisha usambazaji wa umeme vijijini.

"Sheria ya misitu sura ya 323 haijazuia upitishaji wa nguzo za umeme katika hifadhi za misitu hapa nchini," amesema Naibu Waziri Masanja

Amefafanua kuwa Kifungu cha 26 cha sheria ya misitu Na. 14 ya mwaka 2002, kimeweka utaratibu kwa taasisi au mtu anayetaka kufanya shughuli mbalimbali ndani ya hifadhi ya msitu na utaratibu huo unamtaka mtu huyo au taasisi kuwa na kibali kutoka kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kinachomruhusu kufanya shughuli husika. 

Aidha, ameeleza kuwa serikali kupitia TFS kwa nyakati tofauti imekuwa ikizishirikisha Wizara za kisekta kukamilisha miradi ya kimkakati ya kupeleka umeme vijijini bila kuchelewa.