Wednesday , 22nd May , 2024

Mkazi wa Nyakato mkoani Mwanza, Bashiri Mohamed (35), amefikishwa mahakamani na kusomewa shitaka la kuzini na mtoto wake wa kuzaa, analodaiwa kulitenda kati ya Septemba 2023 hadi Februari 15, 2024.

Bashiri Mohamed (35) Mwenye Koti Jeusi akiwa anafikishwa Mahakamani Ilemela, Jijini Mwanza

Mshtakiwa huyo amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza na kusomewa shtaka hilo lenye kosa analodaiwa kulitenda kati ya Septemba hadi Februari 15, 2024.

Akisoma shtaka hilo, mwendesha mashtaka wa serikali Mwanahawa Changale amesema kuwa mshtakiwa kwa tarehe tofauti kuanzia katika eneo la Nyakato-Mecco, wilaya ya Ilemela anadaiwa kuzini na maharimu (16) huku akitambua ni mtoto wake wa kumzaa.

Amesema mshtakiwa ametenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 158 (1) (a) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai sura ya 16  marejeo ya mwaka 2022, ambapo hata hivyo mshtakiwa amekana shtaka na kuomba apatiwe dhamana.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mkazi Mwandamizi, wa mahakama hiyo Juma Opudo amemtaka mshtakiwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini wawili watakosaini hundi ya maneno ya Sh 4 milioni kila mmoja na mwingine awe na mali isiyohamishika.

Mshtakiwa amekwama kutimiza masharti ya dhamana kwani barua ya udhamini ya mdhamini mmoja aliyetokea wilayani Magu haikuthibitishwa na Hakimu Mfawidhi wa wilaya yake.