
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limemkamata Jafari Jumune Lutoboka (32) mkazi wa Mafiga Manispaa ya Morogoro kwa tuhuma za kujifanya mtumishi wa Jeshi la Wananchi Tanzania na kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu.
Mtuhumiwa huyo kwa nyakati tofauti alipita maduka mbalimbali na kujifanyaAskari wa Jeshi la Wananchi Tanzania na kuchukua pochi sita na saa tatu, mali alizodai zinafanana na rangi za Jeshi la Wananchi Tanzania na hazistahili kuwepo madukani hapo.
Upelelezi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa Jafari Jumanne Lutobeka alijiunga na Jeshi la Wananchi Tanzania mwaka 2014 na kuanzia kikosi cha 831 Mgulani kasha kupangiwa Monduli chuo cha maofisa na kufukuzwa kazi 2018 akiwa katika kikosi cha Lugalo akiwa na cheo cha Luteni.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limekamata wahalifu wa makosa mbalimbali katika operesheni kwenye wilaya ya Kilombero kuanzia Agosti Mosi hadi Septemba 15, 2025 na kufanikiwa kukamata jumla ya watuhumiwa 36.
Watuhumiwa watano kati yao wamekamatwa na madawa ya kulevya aina ya bangi kiasi cha Kg 4. Watatu wengine wamekamatwa na lita 40 za pombe aina ya Moshi maarufu kama Gongo, watatu wengine walikuwa na mtambo wa kutengenezea pombe aina ya moshi katika kiwanda bubu cha kutengenezea pombe hiyo.
Aidha, watuhumiwa 22 wengine wamekamatwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo kucheza kamari na kuvuta bangi katika maeneo korofi ya Pembezoni mwa mto Lumemo, Muhola, Katindiuka, Mrabani, Viwanja 60, Mbasa na Kibaoni.
Sanjari na kuwashukuru wananchi waliotoa taarifa na kufanikisha kukamatwa kwa Jafari, Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogorolimewataka wananchi kufanya kazi halali badala yay a biashara haramu.