Wakazi wa Kahama mkoani Shinyanga, wamethibitisha kuwa wapenzi wa muziki wa ndani pale walipojitokeza kwa maelfu na kulipamba tamasha la ‘Kili Music Tour’ lililofanyika viwanja vya Halmashauri na kuleta msisimko mkubwa mjini hapo.

Kutokana na mafanikio makubwa yaliyoonyeshwa Kahama mwaka jana, Kilimanjaro Premium Lager haikuwaangusha wakazi wa Kahama na hivyo kupeleka safu makini ya wasanii waliotoa burudani ya aina yake.

Kwa mara ya kwanza tangu kuanza ziara ya muziki inayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager, wanamuziki Hamis Mwinjuma `MwanaFA’ na Ambwene Yesaya `AY’ walivunja historia ya jukwaa hilo wilayani Kahama, kuwa wanamuziki walioimba nyimbo nyingi.

Wanamuziki wengine walioshiriki tamasha hilo la tatu kati ya 10 yaliyo katika ratiba ya ziara ya muziki ya Kili ni pamoja na Shilole, Christian Bella na Rich Mavoko,Weusi.