Tamasha Kili Music 2012, limehusisha washindi walioshinda tuzo za muziki Tanzania, zijulikanazo kwa jina la Kilimanjaro Tanzania Music Awards Winner’s Tour 2012.

Kabla ya Tamasha hili kubwa kutua jijini Dar es Salaam, wasanii hawa wamepita takribani mikoa mitano, huku shughuli za Tamasha zikiambatana na zoezi la kutafuta vipaji ambalo limefanikiwa kuibua vipaji sita ambavyo vilionekana siku ya tamasha la mwisho lililofanyika Dar es Salaam.

Mikoa ambayo Tamasha limepita ni mikoa ya Dodoma, Mwanza, Moshi, Mbeya na Mtwara. Kila mkoa ulitoa mshiriki mmoja chipukizi kwaajili ya zoezi jipya la kutafuta vipaji lililojulikana kwa jina la Kilimanjaro Awards Talents Search. Mkoa wa Dodoma ulitoa washiriki wawili ambao walilingana alama.

Zoezi hilo lenye lengo la kuibua vipaji vya mikoani lilisimamiwa na Majaji wanne, ambao ni Mshindi wa tuzo ya wimbo bora wa Reggae Queen Darleen, wanamuziki wakongwe wa muziki wa Bongo flava, Profesa Jay na Juma Nature pamoja na Henry Mdimu, ambaye ni Mhariri wa Burudani wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited.

Kutoka Dodoma, chipukizi waliopatikana, ambao walishiriki kwenye tamasha hili kubwa na la aina yake ni Issa Dubat na Juma Madaraka, kutoka Mbeya ni neema, kutoka Mwanza ni Christina, kutoka Moshi ni Sungura na kutoka Mtwara ni Nicolaus.

Chipukizi hao kutoka mkoani ndio walifungua tamasha lililofanyika Dar es Salaam na kufuatiwa na washindi wa tuzo za Kili Mwaka 2012, ambao kwa idadi walikuwa 14 kwa jumla.

Wasanii hao ni Diamond ambaye aliyeshinda tuzo tatu mwaka 2012, Ommy Dimpoz ambaye ni msanii bora anayechipukia ambaye pia ameshikilia tuzo ya wimbo bora wa AfroPop, Ally Kiba ambaye ni mtumbuizaji bora wa kiume, na Barnabas Elias ambaye ni msanii bora wa kiume kwa mujibu wa tuzo za Kilimanjaro za mwaka 2012.

Wengine waliopanda jukwaani ni pamoja na Roma Mkatoliki ambaye anashikilia tuzo ya mwanamuziki Bora wa Hip Hop ambaye pia amenyakua tuzo ya wimbo bora wa Hip Hop, Isha mashauzi ambaye amenyakua tunzo ya wimbo bora wa taarab, Suma Lee ambaye anashikilia tuzo ya wimbo bora wa mwaka, Queen Darleen, Kitokololo ambaye anashikilia tunzo ya rapa bora wa bendi, na AT ambaye ana tunzo ya wimbo bora wenye asili ya kitanzania.

Warriors from the East pia watapanda jukwaani wakiwa ni washindi wa wimbo bora wa reggae, The African Stars wana wa kutwanga na kupepeta pia walipanda na tunzo yao ya wimbo bora kabisa uliowahi kutokea msimu huu wa Dansi, Ben Pol alipanda kama mwanamuziki bora wa R&B na Bi Khadija Kopa aliwakilisha kama mtumbuizaji bora wa kike.

Tamasha hili la Dar es Salaam, lilianza saa kumi jioni ambapo kila mtanzania mpenda burudani alitozwa kiingilio cha shilingi za kitanzania 4000 na pia kupatiwa bia moja bure mlangoni.