Serikali kulifuta shirika la Ndege la Fast jet

Jumatatu , 17th Dec , 2018

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga nchini (TCAA) imesema Shirika la Ndege la fast jet kwa sasa halina hali nzuri na limepoteza sifa ya kuendelea na huduma hiyo, hivyo imetoa notisi ya siku 28 ya nia ya kulifuta kabisa shirika hilo.

Pichani, Ndege ya Fast jet.

Akizungumza na wanahabari, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga, Hamza Johari, amesema 'Notice' hiyo inaanza leo mpaka mwezi Januari huku akitoa tahadhari kwa wananchi kutotumia usafiri wa shirika hilo ili kuepuka usumbufu.

"Kuruka angani huko ni hatari sana, sasa unapokuwa hauna 'accountable manager' mtaalamu wa masuala ya ndege, unakuwa hauna sifa tena", amesema Hamza.

Aidha amesema kuwa pamoja na kuzuiwa kufanya huduma nchini, lakini hawatakiwi kuondoka kwakuwa wanadeni, "Mamlaka imezuia ndege hiyo (Fastjet) isiondoke hapa nchini kwa sababu Shirika linadaiwa madeni mengi, TCAA pekee inadai zaidi ya bilioni 1.4".

Akizungumzia tangazo la shirika hilo kutangaza kusitisha safari katika kipindi cha mwezi Disemba hadi Januari, Hamza amesema kuwa wanatakiwa kulipa usumbufu waliosababisha kwa abiria wake.

"Tunaitaka Fast jet ifuate masharti yetu kwanza kusitisha mauzo ya tiketi za abiria na waliopata madhara wafidiwe kwa mujibu wa sheria na pia wahakikishe wanalipa madeni yote", amesema Hamza.

Kabla ya Mkurugenzi wa TCAA kuzungumza, mapema asubuhi ya leo Disemba 17, Shirika la ndege la Fast jet lilitoa taarifa kwa umma iliyosema kuwa, limesitisha huduma ya usafiri kwa mwezi Disemba na Januari kutokana na sababu za kiutendaji.