Jumatatu , 4th Jul , 2022

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana, amewataka watengenezaji wote wa bidhaa za misitu nchini wahakikishe kuwa wanaweka alama inayoonesha bidhaa zao  zimetengenezwa Tanzania yaani "Made in Tanzania" ili bidhaa hizo zijulikane kuwa zimetengenezwa Tanzania.

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana

Balozi Dkt.Balozi Pindi Chana ametoa kauli hiyo wilayani Mufindi wakati wa ziara ya kikazi ya kutembelea kiwanda cha Dazhong Hood, kinachozalisha bidhaa zinazotokana na misitu na kubaini kuwa bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho hazina alama inayoonesha kuwa zimetengenezwa Tanzania.

Waziri Chana amemtaka mmiliki wa kiwanda hicho Bw. Wu Bing ambaye ni raia kutoka China atekeleze agizo hilo na azingatie sheria, kanuni na taratibu za Tanzania. 

Mbali na agizo hilo Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana amepongeza juhudi za uhifadhi wa misitu nchini zinazofanywa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)  na kuitaka taasisi hiyo  ieendelee kushirikiana na halmashauri za wilaya, wadau mbalimbali na wananchi katika jukumu la kuhifadhi misitu, kusimamia viwanda vya bidhaa zinazotokana na misitu ziwe na alama inayo onesha kuwa zimetengenezewa nchini Tanzania.

Kwa upande wake Mbunge wa Mafinga Mjini Mhe. Cosato Chumi amesema  sekta ya misitu ina mchango mkubwa kwa wananchi hasa wa Mafinga kwa kutoa  ajira nyingi na mchango mkubwa kwenye Mapato ya Halmashauri hiyo kwa asilimia 60,  hivyo yeye kama mwakilishi wa wananchi ataendelea kushirikiana  na Wizara katika uhifadhi wa Maliasili hiyo.