
Esther Bulaya
Bulaya amesema kuwa amefanya utafiti kwenye baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Rwanda ambapo amedai kikotoo chake ni 1/480, Uganda 1/500 na Kenya ni 1/480 huku Tanzania kikotoo kikiwa ni 1/580.
"Kusema kikotoo cha Tanzania ni bora kuliko nchi nyingine Afrika Mashariki ni uongo, nimefanya tafiti nimegundua kuwa Rwanda Uganda, Kenya vikokotoo viko chini kuliko vya kwetu, hii hoja iliyotolewa na Mkurugenzi wa SSRA haina mashiko kwa sababu anaongoza taasisi nyeti," amesema Bulaya.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam, Novemba 26 mwaka huu Mkurugenzi wa SSRA Irene Isaka alisema changamoto hiyo inasambazwa na wanachama wachache, pia ni jambo ambalo linaweza kuzungumzika na kuongeza kuwa sheria ambayo imepitishwa inalenga kuifanya mifuko hiyo pamoja ili ilete faida kwa wanachama wake.
“Sheria ya kuunganisha mifuko imeleta usawa wa wanachama, kwa viwango wanavyochangia, kupunguza gharama za uendeshaji, jambo lingine ni kuweka uwiano kati ya wachangiaji na wastaafu, lakini sasa tuna uwiano mzuri, pia sasa hivi hata akifariki mafao yataendelea kwa miaka 3," alisema Isaka