Jumapili , 16th Sep , 2018

Akiwa katika siku zake za mwanzo ndani ya ofisi, mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Daniel Chongolo, jana amefanya ziara katika eneo la Tegeta ambapo amebaini uchafuzi wa mto Tegeta hivyo kuagiza mamlaka zinazohusika kumpa taarifa ya kina juu ya uchafuzi huo.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Daniel Chongolo.

Chongolo alifika Salasala ambayo ni miongoni mwa maeneo ulipopita mto Tegeta na kusema uharibifu ni mkubwa uliotokana na shughuli za kibinadamu, ikiwemo uchimbaji wa mchanga,  jambo ambalo ni hatari kwa wananchi waliopo kandokando ya mto huo.

Baada ya kujionea uharibifu huo, mkuu huyo wa wilaya ameutaka uongozi wa bonde la mto Wami na Ruvu ambao ndio unahusika na kutunza mazingira ya mto Tegeta kumpa taarifa ya kina juu ya uchafuzi huo.

"Hatuwezi kuacha watu wakaendelea kuchimba mchanga huku wakiharibu mazingira na baadae serikali kuingia gharama ya kuhudumia wananchi walioathirika na mafuriko wakati shughuli za uchimbaji mchanga walizifanya wenyewe" alisema.

Pia amesisitiza haiwezekani vyombo vya kusimamia vipo lakini bado mazingira yanaharibika huku akiwataka wananchi kuheshimu sheria na kulinda mito pamoja na mabonde.

Chongolo ambaye ametokea wilaya ya Longido akichukua nafasi ya Ally Hapi ambaye amekuwa mkuu wa mkoa wa Iringa, amebainisha kuwa hivi karibuni atafanya oparesheni ambayo itahakikisha wale wote wanaovunja sheria hawatabaki salama.