Jumatano , 11th Sep , 2019

Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya, ameagiza wahasibu wa Chuo cha Ualimu Moshi pamoja na Wakala wa Benki ya CRDB Wilayani humo, kukamatwa mara baada ya kugundua ubadhilifu mkubwa wa shilingi milioni 78 zilizokuwa zinalalamikiwa na Wanafunzi Chuoni hapo.

Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya

Akizungumza leo Septemba 11 na EATV&EA Radio Digital, DC Sabaya amesema kuwa mara baada ya kukutana na wote waliotajwa kuhusika na upotevu wa pesa hizo ikiwemo Bodi ya Shule, CRDB pamoja na Mawakala wa ELCT SACCOS, aliagiza wakae ili kuweza kubaini na kujiridhisha kiasi halali kilichopotea.

''Tumekubaliana kwamba wahusika wa wizi huo, huyu Muhasibu wa Chuo na yule Wakala watawajibika kulipa hicho kiasi kwa sababu nao watakuwa sehemu ya uchunguzi huo, lakini ili wasiharibu uchunguzi, nimeagiza wote wakamatwe kwahiyo wote wawili wako ndani mpaka wasubiri kesho saa 5:00 Asubuhi, watanipa majibu ya kilichofikiwa na tutaamua namna ya ulipaji wa fedha hizo ili Wanafunzi waendelee kubaki hapo Shuleni'' amesema DC Sabaya.

Wanafunzi wa Chuo hicho waliandamana siku ya Jumatatu ya Septemba 9 na kushinikiza Serikali kuingilia kati sakata la utapeli wa zaidi ya Sh.milioni 75 za malipo ya ada ambazo hazionekani kwenye akaunti ya Chuo.