Jumatatu , 16th Sep , 2019

Kesi ya Kutekwa kwa Mfanyabiashara Mohammed Dewji 'MO' imepigwa kalenda hadi Septemba 30, itakapofikishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, hii ni baada ya upande wa mashtaka kudai kwamba bado unaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine watano, ambao ni raia wa kigeni.

Mohammed Dewji

Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani hapo leo Septemba 16 kwa ajili ya kutajwa, ambapo Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon, ameyaeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahidi  kwamba, watuhumiwa hao wengine watakapokamatwa  wataunganishwa pamoja na mshtakiwa ambaye ni dereva taksi na Mkazi wa Tegeta, Mousa Twaleb, ambaye kwa sasa anaendelea na kesi ili waweze kujibu mashtaka yao mawili yanayowakabili.

Watuhumiwa wengine ambao mahakama ilitoa hati ya kukamatwa ni pamoja na  Henrique Simbine, Daniel Manchice, Issac Tomo na Zacarious Junior wote Raia wa Msumbiji na Phila Tshabalala ambaye ni Raia wa Afrika Kusini, ambapo wakili Wankyo amesema kuwa wanaendelea kuwatafua na hawatosta kuieleza mahakama hatua waliyofikia.

Baada ya kueleza hayo, Wakili wa Utetezi Robert Mtakula, ameuomba upande wa mashtaka kuongeza jitihada za kuwatafuta kwa kuwa mshitakiwa mmoja yupo ndani kwa muda mrefu.

MO Dewji  alitekwa nyara Oktoba 11, 2018 alfajiri maeneo ya Hoteli ya Colleseum, wakati akienda kufanya mazoezi na alipatikana Oktoba 20, mwaka huo huo katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam.