Jumatano , 27th Jul , 2022

Hakimu anayeendesha kesi inayomkabili Mfalme Zumaridi, na wafuasi wake nane ya kujeruhi askari na kumzuia afisa ustawi kutekeleza majukumu, amegoma kujitoa kwenye kesi hiyo baada ya kudai kuwa hakuna sababu ya msingi ya kuacha kuendelea na shauri hilo hivyo akataka shauri hilo liendelee.

Mfalme Zumaridi

Wakili wa serikali Emmanuel Luvinga, ameiambia Mahakama hiyo kuwa Zumaridi na wafuasi wake wapo tayari kupokea uamuzi huo wa Mahakama, ndipo Hakimu Mkazi Mfawidhi Monica Ndyekobora, akaiambia Mahakama hiyo kuwa kutokana na sababu zilizowasilishwa na mawakili wa upande wa utetezi kutokuwa na mashiko haoni haja ya kutoendelea na kesi hiyo.

Baada ya uamuzi huo wa Makahama, mawakili wa upande wa utetezi ulioongozwa na Steven Kitale, ukasema hawataweza kuendelea na shtaka hilo kutokana na matakwa ya kisheria na kuomba kupangiwa tarehe nyingine ili waweze kuwasilisha sababu zao za kutokuwa na imani na Hakimu huyo.