Jumatatu , 5th Sep , 2022

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana, amesema Chama chao kinaridhishwa na mwenendo wa ujenzi wa daraja la JP Magufuli litakalounganisha kati ya Mkoa wa Mwanza na Geita ambalo linajengwa eneo la Kigogo-Busisi.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana, na viongozi wengine wa CCM

Akizungumza wakati akikagua daraja hilo Kinana ambaye yupo katika ziara ya kukagua uhai wa Chama na kuangalia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025, amesisitiza daraja hilo ujenzi wake unakwenda kwa wakati kama ilivyopangwa, hivyo mwaka 2024 nchi itakuwa imepata alama kubwa ya kuwa na daraja refu lenye urefu wa karibu kilomita 3.2.

“Najaribu kukumbuka madaraja mangapi katika Afrika yenye urefu huo kama hili halitwakua la kwanza basi litakuwa katika tatu bora. Hivyo niwapongeze wote wanaoshiriki ujenzi wa daraja hili ndugu zetu wa kutoka Korea, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wajenzi kutoka Kampuni ya China na Watanzania wote wanaoshiriki,” amesema Abdulrahman Kinana Makamu Mwenyekiti CCM.

Kinana akiwa kwenye daraja hilo baada ya kulikagua na kupata maelezo ya ujenzi wake ambao umefikia asilimia 51, amepata nafasi ya kuwasilimia wajenzi wa daraja hilo na kuwapongeza kwa kazi nzuri.

“Mnafanya kazi nzuri sana, mnafanya kazi kubwa na Rais Samia Suluhu Hassan amenituma nije niwasalimie na niwambie kwamba anangojea aje kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa daraja hili litakapokamilika,” amesema Abdulrahman Kinana Makamu Mwenyekiti CCM.

Awali Mhandishi Mshauri wa ujenzi wa daraja hilo Abulkarika Majuto  ameelezea hatua kwa hatua kuhusu ujenzi huo ambapo amesema kwa sasaa umefikia asilimia 51.