Jumatano , 6th Nov , 2019

Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba,  amemuomba Rais John Magufuli, kuingilia kati suala la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kile alichokidai ni kuepusha vurugu na matatizo kwenye uchaguzi huo.

Lipumba ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mwenendo wa shughuli za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaotarajia kufanyika Novemba 24, 2019.

 "Ili kuepusha suala la vurugu kwenye Uchaguzi huu, naomba Rais Magufuli aingilie kati suala hili na wagombea walioenguliwa wapewe nafasi ya kuteuliwa kugombea".

Aidha Profesa Lipumba ameongeza kuwa, "Kitendo cha kuwanyima fomu wagombea wa upinzani sio tu halina tija kwenye ukuaji wa Demokrasia, pia ni matumizi mabaya na hela za umma, huwezi ukafanya semina, kuchapisha nyaraka mbalimbali huku ukijua hakuna uchaguzi bali wagombea wanapita bila kupingwa".

Hivi karibuni akizungumza jijini Dodoma, Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo, alivitaka vyama vyenye malalamiko kuhusiana na zoezi hilo la Uchaguzi, kufika kwenye ofisi husika kuwasilisha mapingamizi yao.