'Lissu alijitakia mwenyewe, acheni kiburi' -Ndugai

Jumatatu , 9th Sep , 2019

Spika wa Bunge la Tanzania, Mh. Job Ndugai amewaonya wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuacha tabia ya kuwa na kiburi, ujeuri, kujiamlia mambo bila sababu za msingi ili wasiingie matatizoni bila sababu za msingi.

Spika wa Bunge la Tanzania, Mh. Job Ndugai na Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki Tundu Lissu.

Mh. Job Ndugai amesema hayo Bungeni leo, wakati akitoa maelezo kwa Bunge hilo baada ya mahakama kuu nchini kutupilia mbali kesi ambayo ilifunguliwa na Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki kupinga uteuzi wa Mh. Miraji Mtaturu.

Amesema, ''wabunge wanatakiwa kuheshimu sheria na kanuni za Bunge ambazo zimewekwa kwakuwa ndio mwongozo wa shughuli zote za bunge pamoja na uhalali wa wao kuwa bungeni''.

Mh. Ndugai pia amesema anashangaa kuona wabunge hawatoi taarifa wakiwa na changamoto za kiafya na kifamilia, wakati wakijua kikanuni ni kosa kisheria hivyo, maamuzi ambayo yamekuwa yakifanyika hayamwonei mtu.

Hata hivyo, mapema hii leo mahakama Kuu, imetupilia mbali kesi ambayo ilifunguliwa na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Singida Mshariki Ndg. Tundu Lissu la kuomba mahakama hiyo kutengua ubunge wa Mh. Miraj Mtaturu.