Afisa Mtendaji huyo wa Umoja Switch Bw. Danford Mbilinyi akizungumza na wanahabari Jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi inayojihusisha na uunganishaji wa mifumo ya malipo Bw. Danford Mbilinyi, amesema hayo leo huku akishauri serikali kuwekeza katika uunganishaji wa mifumo ya malipo na hatimaye kuachana na uchumi wa malipo ya fedha taslimu, utaratibu aliodai kuwa ni wa gharama na unaozorotesha kasi ya ukuaji uchumi.
"Kwa muda mrefu Tanzania kama nchi tumekuwa tukitumia mfumo wa pesa taslimu katika kulipa huduma na malipo ya bidhaa na huduma, mfumo huu ni wa gharama mno na unaochelewesha ukuaji wa uchumi,..imefika wakati sasa tuunganishe mifumo ya malipo ili malipo yote yafanyike kidijitali," amesema Mbilinyi.
Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji huyo wa Umoja Switch, mifumo ya malipo inayoweza kuunganishwa na kurahisisha malipo ya bidhaa na huduma kuwa ni pamoja na mabenki, kampuni za simu, maduka ya bidhaa pamoja na kampuni za huduma ambapo mteja anaweza kuunganishwa na mifumo yote hiyo katika kifaa kimoja na kuweza kupata huduma pasipo kuhitaji kubeba pesa taslimu.
Mbilinyi amesema kupitia unganishaji wa mifumo ya malipo, huduma za kifedha zitasogezwa hadi maeneo ya vijijini mahali ambako benki na taasisi za kifedha haziwezi kuanzisha matawi yao, na hivyo kuwezesha idadi kubwa ya Watanzania kutumia huduma za kibenki, kupitia miundombinu ya kama mashine za ATM ambazo zimeanzishwa kwa ushirikiano baina ya mabenki na taasisi za kifedha.
Bw. Mbilinyi ameongeza "Kuna maeneo nchini hususani vijijini hakuna kabisa huduma za kibenki. Na hii inatokana na uwezo mdogo wa kila benki kuwa na tawi lake, lakini kwa kutumia mfumo mmoja uliounganishwa, kila benki na taasisi ya kifedha inaweza kujikuta ikitoa huduma katika maeneo ya vijijini tena mahali pasipo na tawi lake".
"Uunganishaji wa mifumo ya malipo una faida kubwa sana kwani mbali ya kukuza uchumi, uunganishaji huo pia utasaidia kudhibiti vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa pesa za umma kwani ni rahisi kufuatilia nani aliyeruhusu malipo hayo, kiasi gani, kwenda kwa nani, kwa ajili ya kugharamia nini," aliongeza Bw. Mbilinyi.
Afisa Mtendaji huyo wa Umoja Switch amesema uchumi wa Tanzania kwa sasa unakuwa kwa kiwango cha asilimia sita nukta tisa hadi asilimia saba, kiwango hiki cha ukuaji wa uchumi ni kikubwa na kinaweza kuongezeka hadi tarakimu mbili iwapo tu kutakuwa na nia ya dhati ya kuwekeza katika uunganishaji mifumo ya malipo.