Jumatano , 11th Dec , 2019

Hatimae kijana Merald Abraham, aliyekuwa amefungwa kwenye Gereza la Ruanda, mkoani Mbeya na kukataa kurejea Uraiani, baada ya kupata msamaha wa Rais Magufuli, tayari ndugu zake wamekwishamchukua na kuondoka naye nyumbani.

Kijana Merald Abraham aliyegoma kurudi Uraiani.

Akizungumza leo Desemba 11, 2019, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mathias Mkama, amesema kuwa kijana Abraham anaonekana hayuko sawa kiakili, kutokana na yeye kukaa gerezani kwa muda mrefu.

"Raia huru yeyote ana Uhuru wa kuzungumza chochote, lakini ninachokijua kwamba huyo hakuwa mfungwa tena bali ni raia mwema, tulitoa huduma baada ya kujijeruhi na kuangalia kama ana tatizo jingine, huyu mtu amekuwa na akili inayobadilikabadilika inawezekana ni kutokana na kukaa gerezani muda mrefu au athari zake kutokana na matendo yake, kiufupi huyu raia hayupo gerezani ndugu zake walikuja kumchukua na wameelekea kwao Mwakaleli" amesema Mkuu wa Magereza.

Kijana Merald Abraham, alizua taharuki siku ya jana ya Desemba 10, 2019, baada ya kugoma kurejea Uraiani kwa kile alichokieleza kuwa hana pa kwenda na kuomba kama ikiwezekana ahamishiwe katika Gereza Kuu la Ukonga, Jijini Dar es Salaam.