Jumatatu , 28th Nov , 2022

Waziri wa TAMISEMI, Angellah Kairuki, ameagiza TAKUKURU kuchunguza matumizi ya shilingi milioni 470, zilizotolewa na serikali kujenga shule mpya ya Sekondari Mwanduitinje, iliyopo jimbo la kisesa wilaya ya Meatu, ambapo fedha hizo zimeisha kabla ya mradi kumalizika ujenzi wake.

Mbunge wa Kisesa Luhaga Mpina

Waziri Kairuki ametoa agizo hilo baada ya kufika shuleni hapo akiwa katika ziara yake ya kikazi, ambapo Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Miundombinu, Maendeleo ya Miji na Vijijini Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Mwita Joram, aliiomba serikali nyongeza ya fedha shilingi milioni 264 ili kukamilisha mradi huo, hali iliyoonesha kumshtua Waziri huyo na kuagiza uchunguzi ufanyike haraka ndani ya siku saba kubaini kama kuna ufisadi.

"Tunachotaka majengo haya yakamilike, hatuwezi tukawa tumemwaga hela yote halafu tukayaacha hivi, ndiyo maana nikasema hebu Afisa wetu wa TAKUKURU aingie kazini kwa siku saba na nitaomba hiyo ripoti inayojitegemea, halafu na Mkaguzi wetu Mkuu wa Ndani na yeye pia aweze kufanya uchunguzi ," ameagiza Waziri wa TAMISEMI.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina, amesema mkwamo wa mradi huo unawaathiri wanafunzi wanaotembea umbali wa kilomita 17 kwenda shuleni, hivyo ni muhimu hatua za haraka zichukuliwe ili Januari 2023, shule hiyo ianze kazi mara moja.