Jumapili , 7th Jul , 2019

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema bado Serikali ina imani na kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania Emmanuel Amunike, na kueleza kwa sasa wamempa mda zaidi kwa ajili ya kuiandaa timu ya taifa ya Tanzania kuekelea michuano ijayo ya CHAN.

Waziri Mwakyembe ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukutana na kufanya naye mazungumzo.

Waziri Mwakyemba amesema kinachohitajika hivi sasa ni suala la muda tu kwani amemueleza mipango mikubwa ya kiufundi aliyonayo kwa timu ya taifa, ili iweze kufanya vizuri katika mashindano yajayo.

Nimefurahi kukutana na kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania, ambapo lengo la kukutana naye ni kunieleza kilichotokea kule Misri katika mashindano ya AFCON, mashindano yamebeba uzito wa kipekee kwa nchi yetu, niseme tu kwamba nina imani kubwa sana na kocha Amunike kuendelea kufanya vizuri na timu yetu", amesema Mwakyembe.

Nimeongea naye mambo mengi sana kuhusu mashindano na tumeona kama Wizara tumpe muda zaidi kwa mipango mizuri ya kiufundi aliyonayo kwa timu ya taifa ili iweze kufanya vizuri katika mashindano yajayo”, ameongeza.

Aidha Mheshimiwa Mwakyembe amesema Kocha Amunike amependekeza mazoezi zaidi kwa wachezaji wa Timu ya Taifa pamoja na kucheza mechi za kirafiki kimataifa mara Tatu kwa Mwaka hili kuweza kupata uzoefu zaidi katika mashindano ya kimataifa.

“Tatizo lililojitokeza ambalo mwalimu anadhani linaweza kutatuliwa ni mazoezi kwa timu ya Taifa, kwamba angalau mara tatu timu ya Taifa kila mwaka ikawa na mechi za kirafiki, wanaitwa leo wanacheza na Zambia, na Afrika Kusini, tungewakaribisha pengine Spain wanakuja na kuangalia mbuga za wanyama, tunajenga imani ya wachezaji wetu".