Polisi wakiwa nje ya chuo cha SAUT Mtwara
Akizungumza na EATV Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi CUF Bw. Julius Mtatiro, amesema mkutano huo ulioandaliwa na Jumuiya ya Vijana wa chama cha CUF mkoani Mtwara (JUVICUF), na Maalim Seif kuwa mualikwa kwenye mkutano huo, na walishapewa kibali na Jeshi la Polisi, lakini leo asubuhi wakiwa kwenye maandalizi, polisi walienda kuzingira eneo hilo na kuwataka wapambaji waondoke, huku wakiwapa taarifa viongozi wao kuwa mkutano huo hauruhusiwi kufanyika tena.
"Mkutano ulikuwa ni wa ndani wa chama, lakini kutokana na mtafaruku uliopo ndani ya chama chetu, tukaona ni busara tukiwajulisha polisi na kuomba ulinzi pia, polisi walituruhusu kuendelea, mkutano wenyewe uliandaliwa na Jumuiya ya Vijana wa CUF na kumualika Katibu Mkuu, sasa leo wapambaji wakati wakiwa kule ukumbini wakipamba, wakafuatwa na polisi wakazuiwa na kuondolewa pale ukumbini, viongozi wakapigiwa simu waende polisi wakapewa barua hiyo ya kuzuiwa, tukiuliza wanasema kwa sababu za amani, pia wakasema Katibu wa wilaya hana taarifa wakati tulisha malizana naye tangu jana", alisema Julius Mtatiro.
Mtatiro aliendelea kwa kusema kuwa walijaribu kuwasiliana na viongozi wa ngazi za juu wa polisi ili kujua kulikoni, na kuambiwa kuwa taarifa iliyopo ndiyo hiyo hivyo lazima ifuatwe.
"Tulimtafuta hadi IGP Mangu ili kujua kulikoni, akatuambia uamuzi lazima ufuatwe, hivyo mkutano hautafanyika", alisema Mtatiro.
Mtatiro aliendelea kwa kuelezea kushangazwa kwake na kuzuiwa kwa mkutano huo, ikiwa siku za hivi karibuni Prof. Lipumba alikuwa mkoani humo na kufanya mkutano bila kikwazo chochote, huku akisindikizwa na boda boda alipokuwa akipokelewa.
"Lakini Lipumba alipokuja huku alipokelewa, tena kwa mapiki piki na watu wengi, akafanya mkutano wa kuongea na wanachama kama wa hadhara, lakini sisi tulikatazwa hata piki piki zisiwepo", alisema Mtatiro.
Mtatiro alisema kuwa polisi hao hawakuishia kuzingira maeneo ya chuo hiko tu, kwani walikuwepo mpaka kwenye hoteli ambazo viongozi wa chama hicho walifikia.



