
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa siku 5 kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Adolf Faustine Mkenda kuondoa tofauti zao vinginevyo atatengua uteuzi wao.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 31 Desemba, 2019 alipokuwa akizungumza na Maafisa na Askari Wanyamapori na Hifadhi ya Misitu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo ambako ametembelea na kujionea vivutio vya utalii.
Katika salamu zake, Mhe. Rais Magufuli amelipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kazi nzuri ya uhifadhi, kukuza utalii na kuchangia mapato ya Serikali lakini ameelezea kusikitishwa kwake na mahusiano mabaya yaliyopo kati ya Waziri Dkt. Kigwangalla na Katibu Mkuu wake Prof. Mkenda hali ambayo inasababisha baadhi ya shughuli za wizara kusuasua.
“Ninafahamu watendaji wenu wa juu, Katibu Mkuu na Waziri kila siku wanagombana, na ninawatazama taratibu, nilishampa kazi Katibu Mkuu Kiongozi awaite awaeleze lakini wasipobadilika nitawaondoa, hilo ni lazima nilizungumze kwa dhati, siwezi kuwa na watendaji wa kuteua mimi halafu kila siku wanagombana, kuna mambo mengi hayaendi, Katibu Mkuu hamheshimu Waziri na Waziri nae hataki kwenda na Katibu Mkuu, siwezi kuvumilia hilo.
Kwa hiyo nalizungumza hili siku ya leo tarehe 31 ya mwezi wa 12 (2019) kwamba wajirekebishe na ikiwezekana wajirekebishe ndani ya siku 5, wawe wanasalimiana, wanazungumza, mimi ninafahamu nina vyombo ninajua nani hafai zaidi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
BREAKING NEWS : Rais @MagufuliJP ametoa siku 5, kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. @HKigwangalla Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Adolf Faustine Mkenda kuondoa tofauti zao vinginevyo atatengua uteuzi wao. pic.twitter.com/iqq12yjEJA
— East Africa TV (@eastafricatv) December 31, 2019