Jumapili , 2nd Dec , 2018

Rais Dkt. John Magufuli amezungumzia kitendo cha Mbunge wa Monduli (CCM), Julius Kalanga kumuomba apeleke maji jimboni kwake ilihali jimbo hilo limewahi kuongozwa na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa ambaye pia amewahi kuwa waziri wa maji.

Rais Dkt. Magufuli akiwa na Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Akizungumza na wananchi wa Arumeru, ambapo amezindua na kuweka jiwe la msingi wa ujenzi wa visima vikubwa vya maji zaidi ya 20 jijini Arusha, Rais Magufuli amesema kuwa anampongeza Kalanga kwa kuhamia CCM akitokea CHADEMA kwakile alichosema ni kitendo cha kijasiri.

"Kalanga,  Mbunge wa Monduli aliwahi kuniomba maji akiwa CHADEMA, lakini amesahau kuwa Lowassa amewahi kuwa Waziri wa Maji, simsemi mzee wangu namaanisha kuwa uzalendo unaanzia nyumbani, nikupongeze Kalanga kwa ujasiri wako wa kurudi huku, maji utapata", amesema Rais Magufuli

Katika hatua nyingine amewaomba Watanzania kumuombea ili awatumikie vyema, "Muendelee kuniombea ili cheo changu cha Urais kikajenge umoja wa Tanzania, mniombee ili nisiwe na kiburi kwa kutumia cheo changu cha urais, mniombee niwe mtumishi wenu ndugu zangu watanzania".

Awali akizungumza mbele ya Rais, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa amesema mpaka kufikia Juni 2020 miradi ya maji 1801 itakuwa imetekelezwa, miradi hiyo imeelekezwa katika maeneo mbalimbali ya nchi yaliyo na changamoto ya maji ili kuhakikisha lengo la serikali la kuwapatia wananchi maji safi linafanikiwa.

"Miradi hii inatuhakikishia kuwa ifikapo 2020 kupitia ilani ya CCM ambayo inasema watu wote wanaoishi katika mikoa wapate maji kwa asilimia 95, wilaya asilimia 90 na vijiji asilimia 85,"amesema Profesa Mbarawa.

Prof. Mbarawa amesema mradi huo uliozindulia na utakaogharimu shilingi bilioni 520 ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa hivi sasa huku akiwahakikishia wananchi kuwa watapata maji masaa 24 siku saba za wiki.