Jumanne , 24th Mei , 2022

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametajwa katika jarida maarufu duniani la TIME 100 kama moja ya viongozi 100 duniani wenye ushawishi mkubwa kwa mwaka 2022.

Jarida hilo limeeleza kuwa Rais Samia ameingia kwenye orodha hiyo kutokana  na aina ya uongozi wake tangu alipoingia madarakani Machi 2021 ikiwemo mabadiliko makubwa aliyoyafanya kwa kipindi kifupi

Baadhi ya mambo yaliyoelezwa katika jarida hilo ni hatua yake ya kufungua milango ya  mazungumzo na wapinzani wake kisiasa, pamoja na uhuru wa vyombo vya habari

 
Aidha hotuba yake aliyoitoa Septemba 2021 miezi michache baada ya kuwa Rais katika mkutano Mkuu wa Baraza la Umoja wa Mataifa ni miongoni mwa mambo yaliyochagiza jina lake kuwepo katika orodha hiyo 

Jarida hilo limemtaja Rais Samia kama kioo kwa wanawake na wasichana wengi Tanzania na nje ya Tanzania na wengi wamekuwa wakimtazama kama mfano wa kuigwa

Katika orodha hiyo Rais Samia amejumuishwa na viongozi wengine wa kimataifa kama Volodymir Zelenskyy wa Ukraine, Xi Jinping wa China, Vladimir Putini wa Urusi na Joe Biden wa Marekani