Ijumaa , 4th Oct , 2019

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila, Jana Oktoba 3, 2019,alizua mijadala mitandaoni iliyokuwa ikihoji, amepata wapi mamlaka ya kuwachapa wanafunzi viboko,ambapo leo Oktoba 4, amezua balaa jingine baada ya kuwarudisha wanafunzi wote wa kidato cha tano na sita katika shule ya Sekondari

Kiwanja kwa kosa la kuchoma Bweni.

RC Chalamila ameeleza sababu ya kuwarudisha wanafunzi hao makwao ni kutokana na kile kinachodaiwa, waliteketeza kwa moto mabweni yao baada ya walimu wao kuwanyang'anya simu, ambapo amewataka warudi, Oktoba 18, huku kila mmoja akipaswa kulipa kiasi cha Shilingi 200,000 na wale waliokamatwa na simu za mkononi, ameamuru walipe  kiasi cha Shilingi 500,000 na warudi shuleni wakiwa na wazazi wao.

''Kama mnaona mnawashwa kuchoma, nendeni mkachome nyumba za Baba zenu, kutoka sasa nafunga form 5 na 6, mnaondoka kwenda kwenu na ikifika saa tano watu wanang'aang'aa mtakung'utwa kichapo cha kufa mtu na Walimu mnaowafundisha mtaenda likizo kidogo na ninyi wote mtakuja na laki 2 na waliokamatwa moja kwa moja na simu mtakuja na laki 5 na wazazi juu''amesema Chalamila

Akizungumzia suala la kuwachapa viboko wanafunzi hao 14, Chalamila amesema kuwa yeye ndio bosi wa Mkuu wa shule katika mkoa na hivyo anaowajibu wa kutoa adhabu kwa wanafunzi wote wanaoonesha utovu wa nidhamu shuleni.

Aidha RC Chalamila ameongeza kuwa hakuna mwanafunzi yeyote atakayeruhusiwa kuhama shule,hadi pale atakapokuwa amekamilisha kulipa kiasi hicho cha pesa na kuuagiza uongozi wa shule, kuhakikisha ujenzi wa mabweni hayo unaanza mara moja pindi pesa hizo zitakapoingizwa kwenye akaunti ya shule.