
Waziri wa Nishati, January Makamba
Waziri wa Nishati, January Makamba, ametoa hakikisho hilo alipozuru eneo la ujenzi wa kituo hicho cha kupoza umeme kitakachojengwa Wilaya ya Bariadi, ambapo miaka 12 sasa Mkoa wa Simiyu hupata umeme kutoka Mwanza, Shinyanga na Mara hali inayosababisha kukatika mara kwa mara huduma hiyo muhimu katika maendeleo ya nchi
"Umeme unapotea mwingi njiani umbali wa ule waya ni mrefu kuliko ilivyo kitaalamu, na umeme unakuwa siyo wa uhakika kama unapooza. Ndiyo maana kuna shida kubwa sana ya upatikanaji na umeme kukatika haraka," amesema Waziri Makamba.
Amesema kituo hicho kitakachoanza kujengwa mwaka ujao, kitaimarisha huduma ya umeme na kuasisi ajira, uwekezaji na shughuli za kiuchumi kwa jamii ya ukanda huu wa wakulima na wafugaji.
"Kwa hiyo utaona kabisa umeme Simiyu upo katika hali mbovu sana. Kuleta umeme mkubwa wa Kilovoti 220 ni mapinduzi ya kiuchumi eeh katika mkoa huu, kwa sababu mkoa huu una potential, una fursa kubwa sana ya kuchangamkia kwa kiasi kikubwa sana kwenye mapato ya Serikali na uchumi wa nchi," Waziri Makamba amesema.
"Lakini wale wawekezaji wa viwanda ambavyo vilitakiwa vianzishwe katika Mkoa wa Simiyu ambavyo vilikuwa bado havijaanza kwa sababu ya changamoto ya umeme, vitakwenda kuanza na vikianza basi mkoa wetu utapandisha pato na wananchi mmoja mmoja wataweza kuinua uchumi wao," Meneja wa Tanesco Mkoa wa Simiyu amesema.
Wakati hayo yakijiri, baadhi ya wanawake wanaojihusisha na ujasiliamali wa kupika vyakula eneo la Mnazi mmoja Mjini Bariadi, wamesema matumizi ya kuni yamewaathiri afya zao, ambapo Waziri Makamba amewapatia jiko la gesi ili waondokane na adha ya kupikia kuni.