Alhamisi , 25th Nov , 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amesema kwamba katika kuelekea kutimiza miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika, nchi imepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kupunguza kiwango cha umaskini kwa wananchi pamoja na kuongeza umri wa kuishi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Kauli hiyo ameitoa hii leo Novemba 25, 2021, Jijini Dodoma, aliposhiriki mkutano wa 20 wa Taasisi za Fedha nchini ulioandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania.

"Wakati nchi yetu inatimiza miaka 60 ya Uhuru mafanikio makubwa tumeweza kupata, la kwanza nchi yetu ni kati ya nchi 10 za Afrika ambazo uchumi wao unakua kwa kasi, tumeweza kuwa na utulivu wa mfumuko wa bei na utulivu wa thamani ya pesa yetu," amesema Rais Samia.

Aidha ameongeza kuwa "Tumeweza kupunguza kiwango cha umaskini kutoka 28.6% mwaka 2015 hadi 26.2% mwaka 2020, tumeweza kuongeza uhai wa mtu kutoka miaka 50 hadi miaka 66 sasa, kwahiyo sisi ambao tuko kwenye 60 bado tuna tamaa ya kusonga mbele na pengine kwa uweza wa Mungu tukapata mingi zaidi sababu hali ya maisha inazidi kuwa bora zaidi kila kuikicha".