Jumanne , 18th Dec , 2018

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro ametaka watanzania kuthamini uwepo wa rasilimali za Wanyamapori pamoja na uoto wa asili katika maeneo ya hifadhi za taifa, kwa kujenga utamaduni wa kutembelea maeneo hayo ili kujifunza umuhimu na nafasi ya uhifadhi katika mchango wa pato la Taifa.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro

Jerry Muro ametoa wito huo katika kampeni maalumu ya kuhamasisha watanzania kutembelea hifadhi ya Arusha hasa katika kipindi hiki cha mapumziko ya mwisho wa mwaka.

Muro amesema kwamba watanzania wanapaswa kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vilivyopo nchini na kusisitiza kwamba vivutio hivyo havipo kwaajili ya wageni wanaotembelea Tanzania pekee.

"Mnapaswa kutenga muda wa kutembelea vivutio hivyo, ikiwa pamoja na kumshukuru Mungu kwa ajili ya kuzaliwa ndani ya nchi hii" amesema.

Hifadhi ya Taifa ya arusha ni miongoni mwa hifadhi chache ambazo zipo kilometa chache tu kutoka makao makuu ya jiji la arusha huku ikiwa ndio lango kuu la kupanda mlima Meru.