Ijumaa , 20th Jan , 2023

Waziri wa TAMISEMI Angellah Kairuki amesema uchumi wa Tanzania umekua kwa asilimia 4.8 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2022 ikilinganishwa na asilimia 3.8 kwa mwaka 2021.

Waziri Kairuki ameyasema hayo hii leo jijini Dodoma kwenye mkutano wa kutangaza mafanikio ya awamu ya sita mkoa wa Dodoma ambapo alikua akimuwakilisha Makamu wa Rais wa Tanzania Dr Mapngo kama mgeni rasmi kwenye mkutano huo.

"Kulingana na Benki kuu ya Tanzania katika robo ya kwanza ya mwaka 2022 uchumi wa Tanzania umekua kwa asilimia 4.8 ukilinganisha na ukuaji wa 3.8 uliokuepo kwa mwaka 2021, hata hivyo kutokana na mipango kabambe tunatarajia uchumi utakua na kufika zaidi ya asilimia 5." Amesema Waziri wa TAMISEMI Angellah Kairuki wakati akisoma hotuba ya Makamu wa Rais

Kwa upande wake Spika mstaafu wa bunge la Tanzania Job Ndugai ametoa rai kwa wakazi wa Dodoma kufanya kazi ili kuwezesha nchi kupata maendeleo kwani serikali inafanya kila kitu ili kuwawezesha wananchi.

"Yako majukumu ya mtu binafsi, familia na jamii kwa ujumla ambapo haya yakifanyika ndio yanaleta maendeleo, twendeni tunafanye majukumu yetu serikali itatusaidia madawa ya kilimo n.k lakini lazima tuanze sisi wenyewe " Spika mstaafu Job Ndugai.

 

Katika mkutano huo ambao umeuzuriwa na wadau mbalimbali wa jiji la Dodoma viongozi wa vijiji na viongozi wastaafu kwa lengo la kuangazia mafanikio ya ndani ya miaka miwili ya utawala wa Rais Saimia, Waziri mkuu mstaafu Peter Pinda ametoa wito kwa viongozi wa vijiji kuwajibika kwenye maeneo yao ikiwemo kuwashirikisha watu wote katika mipango ya maendeleo inayofanywa na serikali ikiwemo mpango mkakati wa kukuza sekta ya kilimo.

"Kwa  bahati nzuri tumefikia malengo mazuri sana kwenye upande wa kilimo lakini panahitajika nguvu kubwa na mimi nataka nikuombe mkuu wa mkoa tusipo angalia Dodoma litakua jiji lenye maghorofa tu,  lakini inahitajika nguvu kubwa tuwe na mpango mkakati wa kuingia vijijini kule na mpango huo uwe shirikishi watu wenyewe washiriki kikamilifu," amesema Waziri Mkuu mstaafu Peter Pinda 

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa huo Rosemary Senyamule amemshukuru Rais Samia kwa maendeleo ambayo ameiwezesha mkoa huo kuyafikia ikiwemo kuongeza shule za sekondari na vituo vya Afya.

"Katika kipindi cha miaka hii miwili ya rais Samia, bajeti ya sekreterieti ya mkoa na Halmashauri  imeongezeka kutoka Bil.314.9  hadi Bil.372 ongezeko la asilia 18 ambapo limesaidia kuongeza huduma za kijamii na kiuchumi katika mkoa," amesema Rosemary Senyamule, Mkuu wa mkoa Dodoma.