Jumatatu , 6th Feb , 2023

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov anatarajiwa kuwasili katika mji mkuu wa Mali, Bamako leo Jumatatu kwa ziara yake ya pili barani Afrika katika kipindi cha wiki mbili. 

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov (kulia) atakua na ziara ya siku mbili nchini Mali kuanzia leo

Wizara ya mambo ya nje ya Mali imesema Bw Lavrov atafanya mkutano na kiongozi wa junta Kanali Assimi Goïta na maafisa wengine wakati wa ziara hiyo ya siku mbili.

Vuguvugu la Yerewolo, ambalo linatetea uhusiano wa karibu kati ya Mali na Urusi, lilikaribisha ziara ya Bw Lavrov na kutoa wito wa kuwekwa kwa kambi ya kijeshi ya Urusi kaskazini mwa Mkoa wa Gao, tovuti ya aBamako inaripoti.

  Bw Lavrov alitarajiwa kuzuru Mali wakati wa ziara yake barani humo mwezi Januari, lakini badala yake alizuru Afrika Kusini, Angola, Eswatini na Eritrea.

Ushawishi wa Urusi nchini Mali umeongezeka  katika siku za hivi karibuni tangu Desemba 2021.

Bw Lavrov alisema Ufaransa imehatarisha  usalama kwa kuondoa wanajeshi wake kutoka taifa hilo la Sahel, ambalo Mali imeiomba Urusi kusaidia kujaza.