
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii nchini Tanzania, Dkt Seif Rashid.
Hali hiyo kwa mujibu wa Makene, imechangiwa na kukosekana kwa lishe ya kutosha kwa akina mama wajawazito pamoja na watoto wachanga chini ya miaka miwili.
Afisa kutoka asasi ya World Vision Tanzania Bw. Bernad Makene, amesema hayo leo wakati wa mkutano wa kimataifa kuhusu lishe, mkutano unaowakutanisha washiriki kutoka nchi zaidi ya ishirini, chini ya mwamvuli wa Mtandao wa Kutokomeza Utapiamlo na Kuboresha Lishe ujulikanao kama Scaling Up Nutrition au kwa kifupi SUN.
Kwa mujibu wa Makene, idadi kubwa ya watoto wamedumaa kutokana na kukosa lishe bora katika kipindi cha siku elfu moja tangu wakiwa tumboni mwa mama zao, ambapo amesema wadau wa SUN wamekutana ili kujadili na kuona ni kwa namna gani Tanzania na nchi nyingine ndani na nje ya Afrika, zinaweza kupunguza udumavu kwa kuboresha lishe kuanzia kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga.
Makene amesema lishe bora ina mchango mkubwa katika suala la watoto kufaulu na kuwa na akili nyingi wawapo mashuleni na kwamba hata afya ya mtu mzima inategemea sana ni kwa jinsi gani mtu huyo alipata lishe bora wakati wa utotoni.