Alhamisi , 3rd Nov , 2016

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Alexander Mnyeti amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri za Arusha DC na Meru wilayani humo, kuwahamisha waalimu wote ambao ni wake wa vigogo wanaofundisha katika shule zilizopo karibu.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Alexander Mnyeti (Aliyesimama)

 

Mnyeti ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na wakurugenzi pamoja na wenyeviti wa vijiji 157 wa wilaya hiyo kwa ajili ya kuwakumbusha wajibu wao.

Amesema shule nyingi za msingi za vijijini, zinakabiliwa na uhaba wa waalimu wakati shule zilizopo katika maeneo ya mijini wilayani humo zikiwa na idadi kubwa ya walimu na wengi wao wake za vigogo.

Amewataka wakurugenzi kuandika barua za uhamisho na uwe uhamisho maalum wa waalimu hao wa wanawake wa vigogo bila kujali cheo cha mume wake.

Akitolea mfano mkuu huyo wa wilaya amesema amekwenda katika shule ya msingi ya Mariwango wilayani humo na kukuta shule hiyo ikiwa na waalimu nane pekee na zaidi ya wanafunzi 600.

Aidha ameagiza barua hizo za uhamisho ziwe na muda maalum wa kuripoti katika vituo vipya vya kazi watakavyopangiwa na endapo hawataripoti kwa muda uliopangwa watakuwa wamejifuzisha kazi.

Amesema hawawezi kusomeshwa kwa fedha za watanzania na kukataa kuwatumikia na kwamba endapo hawatataka kuhama waache kazi, kwani waalimu wapo wengi watapewa nafasi hizo.

Msikilize hapa:-