Alhamisi , 23rd Mei , 2024

Wamiliki wa wa maduka na wafanyabiashara katika eneo la Mwanjelwa kata ya Ruanda, Kabwe na Iyela Jijini Mbeya wamefunga maduka yao na wanachi kukosa huduma  kwa madai ya kuchoshwa na manyanyaso ya maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

Maduka ya Wafanyabiashara yakiwa yamefungwa

Wakizungumza na EATV Jijini Mbeya mapema leo, Mei 23, 2024 wafanyabishara hao wamedai kuwa maafisa kutoka TRA  wamekuwa wakiwakamata wateja wao na kuwanyang’anya bidhaa licha ya kuwa na risiti za manunuzi.

Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Mkoa wa Mbeya, Musibu Shaban amedai wafanyabiashara hao wamekuwa sio waaminifu kwa kutoa risiti zisizo halali kwa wateja wanaowahudumia na wengine hawatoi kabisa risiti hizo.

Katika hatua nyingine baadhi ya wananchi na wateja waliozungumza na EATV wamesema ili kuondokana na usumbufu huo kwa wananchi ni vyema Serikali ikaketi na wafanyabiashara hao ili kumaliza changanoto zilizopo baina yao.