
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Ugavi wa Umeme nchini Tanesco Mhandisi Felchesmi Mramba amesema bado kuna tatizo la baadhi ya wananchi kuiba miundombinu ya umeme na kusababisha usumbufu wakukosekana kwa huduma hiyo vizuri.
Ameyasema hayo kwenye mahojiano maalumu na East Africa Radio kutokana na kuwepo kwa tatizo la kulipuka kwa baadhi ya transifoma na kukatika umeme mara kwa mara kwa maeneo mbalimbali,hivyo amewataka watanzania waache tabia yakuwaficha wahujumu uchumi wa miundombinu hiyo kwakuwa hali yakukosekana umeme kwa maeneo mengi inaleta hasara kubwa kwa pato la taifa.
Amesema adhabu mbalimbali zimeanza kutolewa kwa wale wanaohusika na kuhujumu uchumi wa nchi kwa kuzingatia amri ya mahakama inavyotaka kulingana na kosa husika na adhabu hizo haziangalii cheo cha mtu.
Amekemea baadhi ya wafanyakazi wa Tanesco ambao sio waminifu kuacha tabia yakujihusisha na wizi wa umeme kwa kuwa wengi wanaokamatwa wanauhusiano mkubwa na badhi ya wafanyakazi wa shirika hilo.

