Jumatano , 11th Dec , 2019

Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala, linawashikilia watu wanne akiwemo Mponjoli Elisha (29), Fadhil Hamadi (24), Waziri Hassan (23) na Abdallah Salehe (20) wote wakazi wa Pugu Bombani kwa kosa la kumbaka binti wa miaka 14 na kumsababishia kifo.

Picha inayoonesha vitendo vya Ukatili.

Akizungumza leo Desemba 11, 2019 na EATV &EA Radio Digital, Kamanda wa Polisi mkoani humo Zuberi Chembela, amesema kuwa tukio hilo lilitokea siku ya Desemba 8, majira ya saa 1:30 jioni, huko Pugu Kajiungeni, wakati binti huyo akiwa kwenye matembezi yake ya kawaida, alivamiwa na vijana hao na kumfanyia ukatili huo.

"Tumewakamata watu wanne na wote wamekiri kuhusika na tukio hilo, taratibu za kisheria zikikamilika tutawafikisha mahakamani, na mara nyingi chanzo cha ubakaji ni tamaa tu ya ngono na waliombaka ni watu wazima ambao wanashughuli zao" amesema Kamanda Chembela.

Binti huyo alikuwa ni Mwanafunzi wa Darasa la Sita, katika Shule ya Msingi Pugu Kajiungeni.