Alhamisi , 3rd Sep , 2015

Wanawake nchini wametakiwa wasikubali kurubuniwa na wanasiasa, bali wauone mwaka huu 2015 wa mabadiliko na kuiweka madarakani serikali sahihi, ili iweze kuwawekea mazingira mazuri ya kufanyia biashara zao, na kuwaboresha sekta ya Afya.

Mke wa mgombe wa nafasi ya Urais wa Chadema, Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, Mama Regina Lowassa

Akiongea na wanawake wa mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, mke wa mgombea , mama Regina Lowassa, amesema wanawake wanapaswa kufanya mabadiliko kupitia masanduku ya kura mwaka huu.

Aidha ameongeza kuwa ili wapate neema ya kuwa na mazingira mazuri ya kufanyia shughuli zao za kibiashara zisizokuwa na wingi wa kodi na ushuru kama ilivyo hivi sasa, zinazowaletea kero na kuwafanya wasiwe na maendeleo yoyote basi ni bora wachague UKAWA ili kuyapata yote hayo.

Kwa upande wao baadhi ya wanawake waliohudhuria kikao hicho, wameiomba serikali ya awamu ya tano itakapoingia madarakani, iwaondoe kwenye adha kubwa ya kufanyia shughuli zao za kibiashara kwenye mazingira yenye miundombinu mibovu licha ya kulipa kodi na ushuru mbalimbali, pamoja na kuangalia namna ya kuwalipa wenyeviti wa serikali za mitaa posho.