Jumanne , 10th Sep , 2019

Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), limetangaza kuanza kwa mitihani ya kuhitimu Darasa la Saba kwa watahiniwa 947,221, huku wavulana wakiwa 451,235 na wasichana wakiwa ni 495,986.

Katibu Mtendaji NECTA Dkt Charles Msonde.

Akitangaza tarehe ya Mtihani huo Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dkt Charles Msonde, amewataka wasimamizi wa Mitihani, wazazi na wamiliki wa shule kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu kwani hawatosita, kuchukua hatua kwa yeyote atakajihusisha na vitendo hivyo, sanjari na kukumbusha umuhimu wa watoto wenye mahitaji maalumu.

''Wasimamizi wahakikishe wanalinda haki ya watahiniwa wenye mahitaji maalumu kwa kuwapa mitihani yenye nukta nundu, maandishi yaliyokozwa pamoja na kuwaongezea muda wa dakika 20 kwa kila saa kwa somo la Hisabati na dakika 10 kwa masomo mengine'', amesema Dkt Msonde.

Aidha kati ya watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani huo kuanzia kesho Septemba 11 hadi 12, watahiniwa 902,262 watafanya kwa lugha ya Kiswahili, huku wengine takribani 44,959 wakifanya mtihani kwa lugha ya Kiingereza.