Ijumaa , 25th Sep , 2015

Watanzania wametakiwa kudumisha amani na utulivu katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu ili waweze kuwachagua viongozi bora watakaowaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Shekhe na Kadhi mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Shaaban.

Rai hiyo imetolewa na Sheikhe na Kadhi mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Shaaban kwenye ibada ya swala ya Eid El Hajj iliyofanyika kwenye msikiti wa Ghadaffi uliopo Mjini Dodoma.

Sheikh Shabaan amesema ni jukumu la watanzania wote bila kujali dini zao, itikadi zao za kisiasa na kidini kudumisha amani na utulivu vilivyopo nchini kwani vikipotea ni gharama kubwa kuvirejesha.

Amesema: "Katika kampeni za uchaguzi mkuu zinazoendelea hapa nchini kuna kauli mbiu nyingi zinazotumika wengine wakisema hapa kazi tu, na wengine wakijiita Movement for Change (M4C) kwa madai kuwa wao ni wanamabadiliko tunataka kauli zote hizi ziambatane na ulinzi wa amani na utulivu wa taifa letu."

Aidha amesema kuwa ni jukumu la kila mtanzania kudumisha amani na utulivu vilivyoko hapa nchini kuanzia ngazi ya familia, kwenye kazi zao na kwa kila jambo wanalolifanya ili maisha yaweze kuendelea bila ghasia.

Viongozi maarufu walioswali katika msikiti huo ni pamoja na mgombea mwenza wa Urais kupitia CCM, Samiah Suluhu Hassani na mkuu wa mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa.